Askofu KKKT ajitosa mjadala wa posho

Sunday, 19 June 2011

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mgeni rasmi katika mahafali ya 40 ya chuo cha Uuguzi Machame,mbunge wa jimbo la Hai,Freeman Mbowe akizindua bweni la chuo hicho.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 40 ya chuo cha uuguzi Machame,Mh Freeman Mbowe katikati akiimba wimbo wa taifa,kushoto kwake ni Baba askofu wa KKKT dayosisi ya kaskazini Martin Shao na kulia kwake ni kaimu mkurugenzi wa hospitali ya Machame,Masawe.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 40 ya chuo cha uuguzi Machame,Mh. Freeman Mbowe akihutubia wananchi.
Baba askofu wa KKKT dayosisi ya kaskazini Martin Shao akihutubia wakati wa sherehe za mahafali ya 40 ya chuo cha uuguzi Machame.
Wahitimu.
Wazazi na wageni mbalimbali walifika kuhudhuria sherehe ya mahafali ya 40 ya chuo cha uuganga na uzinduzi wa bweni uliofanyika mwishoni mwa wiki katika hospitali ya Machame.

Na Dixon Busagaga,Hai.

KANISA la Kiinjili la Kilutheria Tanzania (KKKT) limeunga mkono hoja ya wabunge wa kambi ya upinzani kutaka wabunge na wafanyakazi wa kada za menejimenti za utumishi wa umma kutolipwa posho zisizo na tija na badala yake zipelekwe kwa matabibu,wauguzi na walimu wanaofundisha katika mazinira magumu vijijini.

Askofu wa kanisa hilo dayosisi ya Kaskazini Dkt Martin Shao aliyasema hayo katika mahafali ya 40 ya chuo cha uganga machame wilayani Hai yaliyokwenda sanjari na uzinduzi wa bweni la chuo cha uuguzi na harambee ya kuchangia ujenzi wa majengo ya chuo hicho.

Dkt Shao alisema wanaunga mkono juhudi za wabunge hao na kwamba ni vyema posho hizo zikatumika kuboresha maisha ya wafanyakazi wa kada za chini wakiwamo madaktari, wauguzi, wataalamu wengine wa elimu na wahudumu wa ofisi.

“Nchi hii kuna uozo ulioko huko wa kutanguliza mambo binafsi,umimi kwanza ,mimi naunganika na wale wanaosema posho hizo ziende zikasaidie maeneo mengine na wenzetu wanaotoa huduma kwa wengine katika mazingira magumu”alisema askofu Shao.

Dkt Shao alienda mbali zaidi huku akinukuu vifungu katika biblia,ambapo katika kitabu cha Wafilipi 2;3,4, alisema yapo maneno yanayosema “Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno bali kwa unyenyekevu ,kila mtu na amuhesabu mwenzie kuwa bora kuliko nafsi yake.

Aliongeza kuwa katika mstari wa nne katika kitabu hicho kinaendelea kusema kuwa kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe bali kila mtu aangalie mambo yaw engine huku akiwataka waheshiwa kushughulika na mambo ya wengine bila kutanguliza ubinafsi.

Aidha askofu Shao aliiomba serikali kupanga madaktari bingwa na wauguzi katIka hospitali za vijijini kwani asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijiji hivyo wanahitaji huduma kikamilifu kwa kuwa ni haki kupata huduma hizo.

Aliwataka wauguzi kuacha tabia ya kutanguliza maslahi binafsi katika utoaji wa tiba bali kuzingatia viapo vyao jambo ambalo litawajengea heshima na utoaji wa huduma bora huku serikali na wadau wengine wakijitahidi kufikiri namna ya kuboresha maslahi yao.

Kwa upande wake mbunge wa Hai,Freeman Mbowe aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo alisema suala la Posho linaweza kuwatoa roho maana wamegusa mahali pabaya lakini hawaogopi kuendelea na mapambano kuhusu kupunguzwa kwa posho kwa kada mbalimbali za uongozi.

Alisema kwa mujibu wa uchunguzi aliofanya, nchi inatumia zaidi ya bil 912 kwa ajili ya kulipana posho kwa viongozi wa kada zote za utawala lakini kada nyingine zinaendelea kuwa masikini.

“Kilio chetu ni posho ambayo wanaonufaika ni viongozi wa ngazi za juu pekee ,huku wafanyakazi wa ngazi za chini kama walimu, wauguzi, madaktari,wahudumu wa ofisi,madereva na wengine ambao hawana uwezo wa kuitisha vikao hivyo wakiendelea kuwa masikini.”alisema Mbowe.


Hata hivyo alisema kambi ya upinzania haina pingamizi na Posho ya kujikimu ya 80,000 na ile ya kusafiri nje ya nchi wanazolipwa wabunge kwani ni halali,lakini tatizo lao posho hata kwa kazi ambazo hazipaswi kulipwa kwa kuwa ni sehemu ya wajibu.


Katika harambee ya ujenzi huo zilichangwa zaidi ya Sh mil 44 zikiwemo fedha taslimu na ahadi ambapo mbunge huyo alichangia Mil 10 huku kiasi kinachohitajika ni Mil 70.

0 comments:

Post a Comment