MASHABIKI WAWAPIGA SIMBA SC..

Sunday, 19 June 2011

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
JITIHADI za kikosi cha Simba kutaka kusonga mbele na kuweka rekodi kwenye michuano ya Afrika zilikwama jana baada ya kufungwa mabao 2-0 na DC Motemba ya DR Congo katika mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Michuano ya Kombe la Shirikisho.


Pamoja na hivyo, mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu kubwa huku mashabiki wakitumia muda mwingi kurusha chumba na mawe uwanjani hali iliyofanya mkuu wa msafara, Muhsin Balhabou ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya TFF kuwasilisha malalamiko yake kwa kamisaa wa mchezo huo.


Vurugu hizo za watu wa DC Motema Pembe ambayo ililala kwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam zilianza mapema hata kabla ya kuanza kwa mechi baada ya kumvua nguo mwandishi Asha Kigundula wa gazeti la Jambo Leo kwa madai ya kumkagua kama ana hirizi.


Viongozi wa Motema Pembe walimvua Asha nguo wakati akienda chooni. Kwa kushirikiana na askari polisi walimshinikiza kufanya hivyo wakati wote ni wanaume, kitu ambacho kamisaa amekubali kuwa ataripoti kwa Caf.


“Kweli wamenivua nguo, wamenidhalilisha na hawajanikuta na chochote. Viongozi wa Simba na TFF wanalishughulikia suala hilo,” alisema Asha.


Vurugu zilizidi kuwa kubwa baada ya mechi kwisha kwa mashabiki kuvamia uwanjani hapo na kulazimisha maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini DR Congo kuingilia kati na kuwahifadhi wachezaji wa Simba uwanjani hapo kwa zaidi ya saa moja.


“Tunalazimika kubaki ndani ya uwanja, hali ni mbaya. Vurugu ni kubwa na watu hawa wanataka kutuua. Kama tungeshinda nakuambia tungekufa, sijaona watu wasiyo wastaarabu kama hawa.


Askari wanawaangalia tu, kweli Congo hakuna serikali. Wametutupia mawe, chupa tokea mechi inaanza,” alisema Balhabou, kiongozi wa msafara.


Aliongeza: “Kamisaa ameona na ameandika kila kitu kwa kuwa tangu mwanzo wa mechi walikuwa wakiturushia mawe uwanjani.”


Matokeo hayo ya jana yameitoa Simba kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 na kufanya izikose Sh milioni 250 kama ingevuka hadi hatua ya makundi.


Katika mchezo huo, Simba ilijitahidi kulinda lango katika dakika za mwanzo lakini kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele ndivyo ilivyokuwa ikipwaya katika safu ya ulinzi hadi iliporuhusu bao katika dakika ya 38 lililofungwa kwa kichwa na Bokota Labama.


Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, lakini walikuwa Motema Pembe waliopata bao la pili dakika ya 66, kupitia Tresor Salakyaku. Bao hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Simba walioshindwa kuondosha mpira haraka katika eneo lao la hatari.


Pamoja na Simba kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kusawazisha mabao hayo, safu ya ulinzi ya Motema Pembe ilikuwa imara kuhakikisha hairuhusu madhara yoyote langoni kwake na kufanya matokeo hayo kudumu hadi mwisho wa mchezo.

0 comments:

Post a Comment